Jifunze Kilimo Bora Cha Vitunguu-2
Habari rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu karibu tena katika siku nyingine ambapo tunapata nafasi ya kujifunza juu ya fursa ya uwekezaji katika kilimo cha vitunguu lakini ikiwa ni makala ambayo tuliianza wiki iliyopita.
Katika makala hiyo ya wiki iliyopita tuliweza kuangalia aina za kilimo cha vitunguu, mahitaji muhimu katika kutayarisha shamba, upandaji wa mbegu za vitunguu, matunzo ya vitunguu, namna ya kupata mbegu bora pamoja na aina za vitunguu vinavyolimwa nchini kwa wingi.
Leo katika makala yetu, tutaendelea na kuangalia katika maeneo mengine muhimu yanayohusika katika suala zima la uzalishaji wa vitunguu na kukupa faida inayotakiwa ikiwa wewe ni mkulima uliyepania kufanikiwa. Kwa kuanza makala yetu, tutaanza na kujifunza magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
SOMA; Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu
Magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.
Wadudu waharibifu.
Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao hili:
1.Viroboto wa vitunguu.
Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.
Dalili za kugundua.
Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.
Kuzuia.
Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile thiodan-35, Parathion nk. Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako liwe limekomaa.
Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k. Wadudu wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi. Hawa hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.
2. Chawa wekundu. (Thrips)
Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu. (Thrips) ambao wanashambulia majani, Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu.
Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
· Kuweka shamba katika hali ya usafi
· Kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
· Kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
3. Sota (cutworms)
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu
unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao.
Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya usafi.
SOMA; Kilimo Bora Cha Pilipili Hoho Na Faida Zake.
4. Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.
Njia ya kudhibiti:-
· Kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
· Kuteketeza masalia ya mazao
· Kutumia mzunguko wa mazao
5. Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya dhibiti:
· Kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
· Kuteketeza masalia ya mazao
· Kutumia mzunguko wa mazao
Magugu.
Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen
(Goal 2E).
Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.
Magonjwa ya vitunguu.
a) Ukungu mweupe
Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.
Dalili za kugundua Ugonjwa huu
· Utaona unga wa rangi ya zambarau katika majani.
· Majani hugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kunyauka.
· Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia
· Inashauriwa kubadili aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa mwingi.
· Tumia dawa za kuzuia ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k. Wakati unapoona hali ya hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.
b) Ukungu wa kahawia
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.
Dalili zake
Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.
SOMA; Badili Maisha Yako Kwa Kuwekeza Kwenye Kilimo Hiki Cha Vitunguu Saumu.
Namna ya kuzuia
Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa ugonjwa.
· Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.
· Tumia kilimo cha kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.
· Wakati wa kuvuna, epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea na siyo kwa kuchimba na jembe.
· Baada ya kuvuna anika vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au ghala.
c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka. Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au mche mzima hunyauka.
Kuzuia
· Tumia kilimo cha kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja hadi mwingine.
· Panda aina za vitunguu zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red creole.
Kumbuka tumejifunza kuanzia utayarishaji wa shamba na aina za mashamba, pili tukaangalia aina za mbegu na jinsi ya kuchagua mbegu bora yenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa, pia tukalenga kwenye maeneo na hali ya hewa, tukaangaza na katika Magonjwa yanayoweza kuathiri zao la kitunguu pamoja na kudhibiti wake.
Tunakutakia kila la kheri katika kilimo bora na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.
Makala hii imeandikwa na mtaalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji ndugu Mosses Shio Wa TANaGRI.blogspot.com
Jifunze Kilimo Bora Cha Vitunguu-2
Reviewed by Unknown
on
4:21:00 PM
Rating: 5
No comments: