Hatua Nne Za Kukua Kwa Biashara Yako
Ili biashara yako iweze kukua na kukupa mafanikio ni lazima ipitie katika hatua nne muhimu. Hizi ni hatua ambazo biashara yoyote ile, ili iweze kuleta mafanikio, ni lazima ipitie hapo bila kuruka hata hatua moja.
Kama ulivyo umuhimu wa hatua za malezi kwa mtoto kuanzia kutambaa hadi kukimbia na pia hatua hizi ni muhimu katika mafanikio ya biashara hivyohivyo. Ikiwa ikatokea hatua moja imerukwa ni rahisi kwa biashara husika kupoteza mwelekeo au kufa kabisa.
Mpaka hapo bila shaka utakuwa umeona ni kwa jinsi gani hatua hizi zilivyo za muhimu katika kukua kwa biashara. Ni hatua ambazo zinampa mfanyabiashara uzoefu wa kukua siku hadi siku na kupelekea biashara kuleta mafanikio mkubwa.
Je, hatua hizo ni zipi?
Zifutazo Ni Hatua Nne Za Kukua Kwa Biashara Yako.
1. Hatua ya mbegu (Seed stage).
Katika hatua hii, mara nyingi mjasiriamali anakuwa yupo katika hatua ya kujaribu wazo la biashara yake kama linafanya kazi au la. Ni hatua ambayo humfanya mjasiriamali ajaribu mambo mengi ikiwa pamoja na hali ya kuchunguza soko jinsi lilivyo.
Pia hii ni hatua ambayo biashara kwa namna yoyote ile huhitaji pesa ili iweze kusonga mbele. Kwa kifupi hii ni hatua inayohitaji umakini sana kwa sababu ndio msingi na mwanzo wa mafanikio wa hatua zingine zinazofuata. Ikiwa umakini utapotea hapa ni lazima biashara ife.
2. Hatua ya kuchipua ( Start-up stage).
Baada ya kujaribu wazo lako na kuona wazo linafanya kazi, hatua inayofuata baada ya hapo ni hatua ya kuchipua kwa biashara. Hii ni hatua ambayo sasa unaanza utekelezaji wa wazo lako. Ni hatua ambayo unakuwa unatafuta wateja wako mwenyewe sasa.
Katika hatua hii pia mjasiriamali, ni lazima ujifunze jinsi ya kupata mrejesho kwa wateja wako. Ni lazima ufahamu wateja wako wanataka nini au hawataki nini ili kufanya maboresho. Unapozidi kuwa makini katika hatua hii ni lazima idadi ya wateja wako itaongezeka na biashara itakua pia.
3. Hatua ya kukua ( Growth stage).
Mara baada ya bidhaa zako kuwa sokoni, ikiwa utaona bidhaa zako zinatakiwa kwa wingi, elewa kabisa hapo biashara yako hiyo ina dalili tosha ya mafanikio kwa kukua.
Sasa kaika hatua hii, hiki ndicho kipindi ambacho mjasiriamali anatakiwa kuanza kuangalia ushindani na wafanyabiashara wengine. Ikiwa ikatokea umeweza kumudu vizuri katika hatua hii, basi ni wazi mafanikio kwenye biashara yako ni lazima yaonekane.
4. Hatua ya kukomaa ( Maturity stage).
Hapa katika hatua hii, biashara yako inakuwa imemudu kuweza kukabiliana na ushindani wa kila aina. Hiki ni kipindi ambacho biashara yako inakuwa inajitatanua na kutengeneza matawi katika sehemu zingine tofauti.
Kwa kifupi, hii ni hatua ambayo mjasiriamali anayaona mafanikio yake kwa sehemu kubwa. Lakini hata hivyo ni hatua ambayo mjasiriamali pia hatakiwi kulewa zaidi ya kuendelea kuweka juhudi hadi kufanikiwa zaidi na zaidi.
Kumbuka, hizo ni hatua muhimu nne ambazo biashara yako ni lazima ipitie ili iweze kukua na kukuletea mafanikio. Hata hivyo, hizi ni hatua ambazo zinategemeana sana. Kushindwa kwa hatua moja, ni dalili tosha inayoonyesha pia na hatua zingine zitashindikana kufanikiwa.
Kitu cha kujiuliza wewe upo katika hatua ipi? Kwa hatua yoyote uliyopo itakusaidia kujua kama utafanikiwa au la!
Endelea kutembelea pinesoup.blogspot.com kujifunza kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
Hatua Nne Za Kukua Kwa Biashara Yako
Reviewed by Unknown
on
3:51:00 PM
Rating: 5
No comments: